Tafsiri ya nyama na Aina zake
Katika miaka ya hivi karibuni elimu juu ya ulaji na mitindo ya maisha imepata usikivu wa kutosha kutoka kwa jamii ya wanadamu. Hii limetokea, huenda, kwa sababu ya taarifa za tafiti zinazoonyesha kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukizwa mathalani Sukari, Saratani, Shinikizo la damu n.k.
Neno nyama sio geni kwa yoyote yule aliyekatika umri wa kujitambua ambapo hata mtoto anafahamu nyama ni nini. Lakini, kwa tafsiri ya haraka haraka, Nyama ni chakula kinachotokana na sehemu ya mwili (Msuli) wa kiumbe kundi la wanyama ambalo linaweza kujumuisha samaki, Ndege, Ng’ombe, Mbuzi, Kuku na kadhalika. Nyama zimegawanywa katika makundi mawili, nyama nyekundu na nyama nyeupe.
Nyama nyeupe ni ile nyama inayoonekana kutokua na rangi nyekundu ambayo huonekana kama nyeupe(Tizama picha hago chini kwa kuelewa zaidi). Vyanzo vya nyama nyeupe ni pamoja na Kuku, Bata samaki n.k. Kwa nini nyama hii ni nyeupe.? Kama ilivyolelezwa hapo juu, sababu kuu ni kiasi cha Maadini chuma (Iron, Fe) yaliyopo kwenye damu ya hawa viumbe. Mathalani, nyama ya kuku ina kiasi cha 0.7 mg za madini chuma katika kila 100gm ya nyama ikilinganishwa na nyama ya ng’ombe ambayo ina 2mg za Madini chuma (Fe) kwenye kila 100gm.
Chanzo cha Picha; Shutterstock
Nyama nyekundu ni aina ya nyama inayonekana kuwa na rangi nyekundu na hii hutokana na uwepo wa madini chuma (Iron, Fe) kwenye damu kwa wingi. Mifano ya vyanzo vya nyama nyekundu ni pamoja Ng’ombe, Mbuzi, Kondoo na wanyama zengine wenye miguu minne. Tizama picha hago chini kwa kuelewa zaidi.
Katika makala hii tutajikita katika kujadili mbichi na mbizu za kula nyama ya Nyeupe hasa hasa ya nyama ya kuku.
Chanzo cha Picha; Delighted Cooking
Ni faida zipi mtu hupata atumiapo Nyama nyeupe ?
Mosi, Ni nyama yenye mafuta kidogo na salama kwa Afya ya Binadamu
Kwanini nyama hii inatajwa kuwa na kiasi cha mfuta kidogo ?, Kwa sababau nyama ya kuku ina mafuta (fats) kiasi kidogo kulinganisha nyama itokanayo na wanyama kama ng’ombe na mbuzi(Nyama nyekundu). Sehemu kubwa ya mafuta haya huhifadhiwa kwenye ngozi ya kuku.
Kiasi cha mafuta atakacho pata mtu kwa mlo mmoja itategemeana sababu kadha wa kadha ikiwemo; Kiasi na sehemu ya mwili aliyokula na ni kwa namna gani nyama imeandaliwa (ngozi ikiwa imeondolewa) au lah).
Mathalani; Nyama ya kidali - ina gramu tatu (3) za mafuta kwenye gramu 100 lakini pia nyama ambayo ngozi yake imeondolewa ina mafuta kidogo sana na kufanya nyama kuwa salama kwa afya ya mwili. Hata hivyo, mafuta yanayopatikana kwenye nyama ya kuku nusu (1/2 au 50%) ni mafuta yanayoyeyuka kirahisi kwenye joto la mwili wa binadamu (unsarurated fats).
Kitu kingine cha faida kuhusu mafuta haya yatokanayo na kuku, ni kwamba hayana kemikali ijulikanayo kama trans fats ikilinganishwa na nyama itokanayo na ng’ombe, mbuzi na kondoo ambayo ina aina hii ya mafuta sumu au mabaya kwa kiasi kingi. Mathalani huko Canada, uchunguzi ulifanyika na kugundua kuwa, 2% hadi 5% ya mafuta(fats) yanayopatikana kwenye nyama ya Ng’ombe na 8% kwenye nyama ya kondooo ina aina hii mafuta mabaya ambayo tunaweza yaita mafuta sumu. Mafuta haya mabaya yajulikanayo kama Trans fats yamekua yakihusishwa na kusababisha magonjwa ya moyo kama ilivyooneshwa kwenye utafiti uliofanywa na kundi la wanasayansi (1).
Je, ni kiasi gani cha nyama nyekundu cha faa kiafya kuliwa kwa siku ?
Kuwepo kwa aina hiyo ya mafuta katika nyama nyekundu inaweza isiwe zuio kwamba usile, la hasha bali nikukujulisha na kukutahadharisha kuwa kama utapenda kula nyama hiyo hivyo basi usizidishe.Kwa mfano, nyama ya Ng’ombe, usizidishe kula zaidi ya nusu kilo kwa juma (500gm/week), wastani wa gramu 70 za nyama kwa siku. Hii ni kwa mujibu wa Tafiti zinazofanywa na Mfuko unaofanya tafiti za magonjwa ya saratani ulimwenguni (The World Cancer Research Fund).
Mbili, Ni nyama yenye kirutubisho omega -3 fat.
Tatu, Ni Chanzo Kizuri Cha Tindikali iitwayo Folic na Seleniamu.
1. Tindikali iitwayo Foliki; Vyanzo vya Foliki (follic acid) vinavyotegemewa sana sana ni mboga za majani zenye kijani kilichoiva, hata hivyo kirutubisho hicho hupotea au kupotezwa wakati wa maandalizi ya chakula na kwa sababu hiyo hupelekea kufanya kiasi kinachofika mzunguko wa damu kuwa kidogo sana na kusababisha upungufu ambao umehusishwa na mambo mengi ikiwemo;
🔺Watoto kuzaliwa wakiwa na uzito chini ya kiwango
🔺Watoto kuzaliwa wakiwa na mgongo wazi
🔺Vifo vya vichanga miezi michache baada ya kuzaliwa
Kiwango cha Folic acid kinachohitajika kila siku (RDI, Required Daily Intake) ni 200µg ambacho kinaweza kupatikana kwa kula 88gm kwa siku za nyama ya kuku ambacho ni kinaweza kupatikana kwakula kipapatio au paja la kuku. Hii inaweza kuwa chanzo kizuri cha follic Acid na kuzuia vifo na ulemavu kwa watoto wachanga.Kiwango hiki cha folic acid kinachopatikana kwenye Nyama ya kuku hakiwezi kupatikana kwenye nyama nyekundu kwa kiasi sawia.
2. Madini ya seleniamu; Vyanzo vizuri vya Seleniamu ni pamoja na; Mboga za majani, Vyakula vitokanavyo na viumbe waishio baharini na nyama/mayai ya kuku. Kirutubisho hiki kinaweza kupatikana kwa wingi kupitia kula nyama ya kuku au ndege yoyote wa kufugwa.Hebu tuzifahamu kazi za seleniamu kwenye mwili wa mwanadamu;
i. Husaidia kinga ya mwili; Husaidia katika kuboresha ufanyaji kazi wa kinga ya mwili na kusaidia mwili pia katika kuzuia Virusi(VVU) vya ukimwi kusababisha ukosefu wa Kinga Mwilini (UKIMWI). Ambapo, tafiti zilizofanyiaka mwaka 2006 huko uingereza, ilionekana kuwa maeneo yaliyo na ardhi yenye kiasi kingi cha madini ya seleniamu, wagonjwa wa UKIMWI walikuwa wachache ikilinganishwa na maeneo yaliyo na ardhi kiasi kidogo au hamna kabisa seleniamu (Jacques, 2006)
ii. Hupunguza hatari kupata saratani ya tezi dume kwa wanaume
iii. Husaidia kwenye Afya ya Uzazi; Huongeza uwezo wa mbegu za kiume kukimbia wakati wa urutubishaji yai (sperm motility) na Kupunguza hatari za utokaji wa mimba ovyo ovyo.
Ni kweli kwamba seleniamu inapatikana ardhini kwa wingi na binadamu hali udongo, hivyo kiasi hiki kingi kinaweza kuongezwa kwenye vyakula walavyo kuku na ndege wa kufugwa pia. Kufanya hivyo hufanya upatiakanaji wa madini haya muhimu kuwa rahisi kwa binadamu kupitia kula nyama ya kuku.
Hivyo basi, kuhitimisha makala hii, nikuombe uitumie elimu hii katika maisha yako ya kila siku ili kuboresha afya na kujikinga na maradhi mbali mbali yatokananayo na ulaji wa nyama. Kwa maoni, maswali (kwa mahali ambapo hujaelewa), mapendekezo na marekebisho usisite kutuachia ujumbe wako hapo chini. Ahsanteni.
Rejea
1. Bingham, S. 2006. The fibre – folate debate in colo-rectal cancer. Proceedings of the Nutrition Society, 65 (1): 19–23.
2. David Farrell, School of Land, Crops and Food Sciences, The University of Queensland, St. Lucia 4072, Queensland, Australia
3. Jacques, k.a. 2006. Zoonotic disease: not just from birds, and not just in the flu. In T.P. Lyons, K.A. Jacques and J.M. Hower, eds. Nutritional biotechnology in the feed and food industries: Proceedings of Alltech’s 22nd Annual Symposium, Lexington, Kentucky, USA. 23-26 April 2006, pp. 149-159. Nottingham University Press, UK
Comments