Utangulizi
Mwezi Aprili ni mwezi wa ufahamu wa Saratani Ulimwenguni kote. Saratani ni moja ya magonjwa yanayotishia Amani ya Mwanadamu na Ulimwengu kiujumla. Kwa miongo kadhaa sasa saratani imekua ikisababisha uremavu na vifo vingi katika jamii. Tafiti mbali mbali zimefanyika kuweza kujua namna ambavyo ugonjwa huanza na Sababu za kutokea kwa aina hii ya magonjwa.
Tanzania, ikiwa kama nchi ya Uchumi wa kati mpaka kufikia mwaka 2018 ilikuwa tayari imetumia takriban Dola za kimarekani Bilioni 2.3 katika mapambano zidi ya magonjwa ya Saratani. Katika Kiasi hicho chote cha Fedha, 24% ya pesa hizo kilikua kimetokea nje ya mfuko wa serikali, 32% kutoka kwa hisani kutoka kwa mataifa marafiki wa Tanzania na 35% Kutoka katika Mifuko ya Watanzania (Bajeti ya Serikali).
Kwa miaka ya hivi karibuni mpaka sasa, Tanzania imekua ikipitia uzoefu mgumu wa ongezeko la wagonjwa na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa saratani. Ambapo mpaka mwaka 2020, kuliripotiwa visa vipya wa wagonjwa saratani 40,464 ambapo katika wagonjwa hao;
· 25% Saratani ya Mlango wa uzazi (Cervical Cancer)
· 10% Saratani ya Matiti (Breast Cancer)
· 09% Saratani ya Tezi dume (Prostate Cancer)
· 5.8% Saratani ya Utumbo Mpana (Bowel Cancer)
· 6.5% Saratani ya Koo la Chakula au umio (Oesophageal Cancer).
Saratani ni Nini na nini Kinasababisha ugonjwa wa Saratani?
Saratani ni ugonjwa wa chembe chembe hai za mwili (seli), ambao hufanya seli kutokufanya kazi zake ambazo seli ikiwa nzima bila madhara inapaswa kuzifanya. Mathalani, chembe chembe hai zinazounda mfumo wa Damu hufanya kazi ya kusafirisha gesi ya oksijeni kutoka kwenye mapafu kuelekea kwenye maeneo mbali mbali ya Mwili. Hivyo basi, chembe chembe hizi zikishaathirika na kugeuka kuwa saratani hushindwa kufanya kazi yake na kuufanya mwili kukosa oksijeni na kupelekea kuwa dhaifu.
Ukiachilia na kupoteza uwezo wake wa kufanya kazi, hizi chembe chembe hai huzaliana kupita kiasi na kufanya ongezeko kubwa la seli zisizo na kazi yoyote mwilini. Kwa baadhi ya sehemu za mwili, Ongezeko hili husababisha kutokea kwa uvimbe ambao hukua na hadi kupelekea kuathri viungo vya mwili vilivyo jirani na uvimbe. Kukua kwa uvimbe hupelekea kudhoofu kwa mwili na hata kupelekea kifo.
Mpaka sasa kisababishi cha Saratani kinaonekana kuwa ni mabadiliko katika Vinasaba (DNA) vya Chembe chembe hai za mwili. Mabadiliko haya hupelekea kubadilika kwa mfumo wa uendeshaji na utoaji taarifa zinazoathiri uwezo na ufanyaji kazi wa Mwili kiujumla.
Nini Dalili za Saratani za Utumbo?
Kabla hatujaangazia dalili za Saratani ya utumbo, nikuombe msomaji uelewe hivi, Baadhi ya wagonjwa wa saratani huwa hawana dalili zozote zinazoashiria saratani lakini wakati wa uchunguzi hukutwa na ugonjwa huu. Lakini pamoja na hayo, baadhi ya wagonjwa hupata dalili zifuatazo;
· Kupata choo chenye damu
· Kupata mchafuko kwenye utumbo ambao huambatana na Kuharisha ama Kupata choo kigumu
· Kupata hisia za tofauti kwenye eneo la utumbo lililo karibu na puru (mkundu) ambalo hujulikana kama rektam.
· Kupata maumivu wakati wa haja kubwa
· Mwili kuchoka na kukosa nguvu.
· Kuziba kwa utumbo ambako hupekekea mgonjwa kukosa choo
· Kushuka kwa kiwango cha chembe chembe hai za damu (RBCs) mwili ambayo hujulikana kama anemia.
· Kubadilika kwa muonekano wa kinyesi na kuwa na mauteute au makamasi kamasi.
· Kupata hisia ya kwenda haja kubwa lakini hakuna choo kinatoka
Hivyo upatapo moja ya dalili zilizotajwa hapo juu, tafadhari usikae nyumbani nakuanza kujitibu na madawa ya kienyeji Nenda Hospitali ukachunguzwe na wataalamu wa Afya.
Nini vihatarishi vya Saratani ya Utumbo?
Kwa tafiti za kitabibu zilizofanyika miaka ya hivi karibuni, zinaonyesha kuwa kunaongezeko kubwa la wagonjwa wa wa saratani ya utumbo ambao umeathiri hasa hasa kwenye majiji ambapo panahusishwa na kuwepo na mitindo ya Maisha isiyofaa kwa kiasi kikubwa(2).
Moja ya changamoto kubwa iliyopo hadi leo kuwa, kisababishi cha moja kwa moja cha Saratani ya Utumbo hakijulikani. Pamoja na hayo, tafiti mbali mbali za kitabibu zimefanyika na kubaini kuwa zifuatazo ni baadhi ya vihatarishi (Risk factors);
vUmri mkubwa; Watu wenye umri mkubwa, umri wa kuaanzia miaka 50 au Zaidi wako hatarini Zaidi kupata saratani hii.
vMagonjwa mbali mbali kwenye utumbo mpana au mdogo
Kuwepo kwa ugonjwa/Magonjwa kwenye utumbo kwa muda mrefu hadi miaka nane (8) huongeza hatari ya kupata saratani hii.
vMtindo mbovu wa Maisha
Mtindo mbaya wa Maisha nayo moja kihatarishi cha kupata Saratani ya Utumbo. Mitindo mibovu ni pamoja kuwa na uzito uliopitiliza, kutokufanya mazoezi mara kwa mara, matumizi ya Pombe, Sigara na ulaji wa vyakula vyenye nyama nyekundu iliyochakatwa viwandani.
vUgonjwa kwenye Vinasaba uliorithiwa
Saratani hii pia inaweza kurithiwa kutoka kwa wazazi na kwenda kwa watoto. Na hii inaweza kuendelea kutoka kizazi kimoja hadi kingine cha Familia hiyo.
vHistoria ya familia
Familia yenye historia ya kuwa na mgonjwa mwenye sartani ya utumbo ipo katika hatari ya mmoja wao kuwa na ugonjwa huu.
vKuwepo kwa vinyama kwenye utumbo (Polyps)
Watu walio na vinyama nyama kwenye utumbo wako katika hatari ya kupata Saratani hii.
Nini kifanyike kupunguza hatari ya kupata Saratani hii?
ØKufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara
ØKudhibiti uzito wa mwili (BMI; 20 - 25)
ØKupunguza au kuachana kabisa na utumiaji wa nyama nyekundu kwa mfano; Nyama ya ng’ombe, mbuzi na zingine zote uzijuazo kuwa ni nyama nyekundu. Mbadala ya hiyo, kula nyama nyeupe ambayo ni pamoja na nyama ya Kuku au ndege, Nyama ya samaki na Nyama itokanao na viumbe wa majini.
ØKula nafaka isiyokobolewa, Vyakula vilivyo na nyuzi nyuzi na vyakula vitokanavyo na maziwa.
ØUtumiaji wa Dawa ijulikanayo kama aspirin mara kwa mara imeonyesha kuwa matokeo mazuri katika kupunguza hatari ya kupata Saratani ya utumbo.
ØKumbuka kumuona Daktari au Mfamasia kuhusu matumizi na usalama wa Dawa hii kabla ya kuitumia.
Je ugonjwa huu unatibika?
Jibu ni Ndio, endapo tu utagunduliwa mapema kabla ugonjwa hauja athiri sehemu au viungo vingine vya mwili na Hautibiki endapo utachelewa kugundulika kuwa una ugonjwa huu. Hivyo nikusihi na kukushauri kufanya uchunguzi wa mara kwa mara kwenye mwili wako kwa kufika katika kituo cha kutolea huduma za Afya kinachotambuliwa na serikali.
Unapogundulika mapema, ugonjwa huu hutibika na hata uwezekano wa mgonjwa kurejea hali ya kawaida(Afya njema) katika shughuli za kimaisha ni kubwa pia.
Ni Vipimo gani vinafanyika kuweza kubaini kama kuna saratani ama la?
Ili kuweza kubaini kama mgonjwa ni ana saratani ya Utumbo, Madaktari huomba moja wapo wa vipimo vifuatavyo kwa kuangalia vigezo mbali;
²Flexible sigmoidoscopy
²Carcinoembryonic Antigen (CEA) blood test
²Computed Tomography (CT) scan
²MRI scan
²Immunochemical faecal occult blood test (IFOBT)
Matibabu ya Saratani ya Utumbo?
Matibabu ya Saratani ya Utumbo mpana huamuliwa kwa kuzingatia hatua saratani ilipofikia ambapo saratani hupitia nne, hatua I, II, III na IV. Hivyo matibabuya wagonjwa ambao wapo katika hatua tofauti wanaweza tofautiana kidogo katika aina ya matibabu na hata dawa zitakazotumika. Lakini pamoja na hayo, Saratani inaweza kutibiwa na moja wapo au matibabu aina mbili au tatu zote kwa kuzingatia tu hatari na faida za kila aina ya Matibabu bila kusahau kuangalia hatua ya ugonjwa. Matibabu yapo katika makundi yafuatayo;
nMionzi (Radiotherapy)
nDawa au Kemikali (Chemotherapy)
nUpasuaji (Surgery)
Katika kuchagua, madaktari bingwa watakushirikisha katika kufanya maamuzi na kuchagua ni matibabu yapi yatakufaa kuainisha faida na hasara za kila aina ya chaguo.
Dawa za Saratani
Dawa za saratani ni moja ya Dawa zenye changamoto nyingi kwani zisipotumika vyema zinaweza kusababisha saratani tena, Ndio maana hurusiwi kujitibi nyumbani pasibo usimamizi wa Madaktari bingwa au Wafamasia Bingwa wa Magonjwa ya Saratani. Dawa hizi zinzaweza kuwa zifuatazo;
lMonoclonal antibodies
lBevacizumab
lOxaliplatin
lCisplatin
lCetuximab and panitumumab
Maudhi au Kero za Dawa za Saratani
Kama nilivyotangulia kuandika hapo juu, Dawa zinazotumika kutibu magonjwa ya saratani huleta maudhui mengi kwa mgonjwa lakini baada ya matibabu maudhi haya huondoka pole pole kadri uda unavyoenda. Hapa chini ni baadhi ya maudhi ya dawa zinazotumika kutibu saratani;
uKichefu chefu na kutapika
uKujisikia mgonjwa
uKuharisha
uKupata michubuko na vidonda ndomoni
uKupoteza hamu ya kula
uKubadilikaje kwa uwezo wa kunusa na kuhisi radha ya Chakula
uKupoteza Nywele ikiwemo za kichwani
uMwili kupungua uzito na kukonda
uKupata gandhi kwenye sehemu mbali mbali za mwili*
uKuhisi kama unachomwa vipini*
uKuvimba kwenye vidole vya miguu na mkononi*
uNgozi kubanduka au kuchunika**
uHisia ya kuungua Ngozi unapopita juani**
uLakini pia mgonjwa akiwa kwenye matibabu ya aina hii kinga yake ya mwili hushuka na kupelekea kuaza kusakamwa na magonjwa nyemelezi
* Maudhi haya hujitokeza hasa hasa kwa dawa iitwayo Oxaliplatin
** Maudhi haya hujitokeza hasa hasa kwa dawa iitwayo Fluorouracil (5-FU)
Wapi matibabu haya hutolewa Nchini Tanzania?
Mpaka kufikia mwaka 2021, Vituo vya kutolea huduma za matibabu ya Saratani vilikuwa
Vinne tu lakini serikali katika kupambana na tatizo hili, hadi kufikia mwaka 2022 vituo vimeongezeka na kufikia sita (6) kama ifuatavyo;
nAga khan Hospital – Dar es salaam
nKilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) - Kilimanjaro
nBugando Medical Centre (BMC) – Mwanza
nOcean Road Cancer Institute – Dar es salaam
nHospitali ya Benjamin Mkapa - Dodoma
nHospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya - Mbeya
Reference:
1. https://www.worldometers.info/world-population/tanzania-population/17:26-05/04/2022
2. L. Katalambula, P. Petrucka, J. Buza, and T. Ngoma; Colorectal Cancer Epidemiology in Tanzania: Patterns in Relation to Dietary and Lifestyle Factors, Journal of Global Oncology 2018 4: Supplement 2, 3s-3s.
Comments