Zifahamu dawa hatari kutumia pamoja na pombe.
Pombe ni nini hasa ?
Habari yako ndugu mpenzi msomaji wa blog yako ya “ZIJUE DAWA
ZAKO”, pia pole na majukumu ya kila siku. Leo napenda kukuletea ya dawa iitwayo
“Pombe”. Pombe ni kundi la kemikali mbali ambazo namna au nyingine zinafanana
kwa matokeo yake, kundi hili linahusisha kemikali kama (majina ya kitaalamu) Ethanol, Methanol
na ethyl glycol. Ethanol ndio inapatikana kwa wingi katika vileo
vingi. Natumaini ulishawahi kukutana na maelekezo yakitolewa na mfamasia au
daktari kwamba usitumie pombe kabisa hadi pale utakapo utakapomaliza dozi yako,
basi karibu tena leo uzijue dawa ambazo hutakiwi kutumia pombe kabisa ukiwa
kwenye dozi.
Najua utashangaa
kwanini pombe nimeiita ni dawa, labda nieleze kidogo kwanini nimeiita pombe
kuwa ni dawa, Pombe ni dawa kwa sababu, utendaji kazi wake ni sawa kabisa na
jinsi ambavyo dawa za usingizi hufanya kazi. Madhara yake baadhi pia nayo
yanafanana na dawa za usingizi. Na pia Pombe aina ya ethanol hutumika kusafishia
vidonda, kusafisha mikono baada ya kusafisha majeraha na kusafishia vifaa kwa
minajili ya kuua vimelea vyovyote ambavyo vyaweza kuwepo pale.
Hebu sasa tuangalie
dawa ambazo hutakiwi kutumia kileo au pombe yoyote uwapo kwenye dozi, Dawa hizi
ambazo tunaenda kuziona hapo chini husababisha madhara ambazo zinajidhihirisha kupitia dalili zifuatayo kama
zikitumiwa pamoja na pombe; Kichefuchefu, kutapika, kizunguzungu, maumivu ya kichwa na Joto na kujaa usoni. Dalili hizi zinaweza kusababisha kifo kama mgonjwa hatawahishwa hospitali kwajili ya kuzishughulikia.
1.
DISULFIRAM, METRONIDAZOLE,
TRIMETHOPRIM NA CEFOTETAN.
Dawa hizi hutumika kutibu matatizo (Magonjwa) mbalimbali ya
mwili zikiwa katika muunganiko na dawa zingine au pekee. Magonjwa yanatibiwa na
hizi dawa ni kama yafuatayo kwa ufupi,
·
Disulfiram
Dawa hii hutumika
kutibu saratani inayotokea kwenye mishipa ya fahamu sehemu ambazo kitaalamu
zinaitwa ganglia. Saratani hii inaitwa Glioblastoma Multiforme.
·
Metronidazole
Metronidazole ni jina la dawa husika ambayo imezoeleka
kuitwa kwa jina la flagyl, Dawa hii husaidia au hutibu magonjwa
yanayosababishwa na wadudu waitwao bakteria. Na pia dawa hii hutumika kuzuia
mambukizi kwa wagonjwa wanaojiandaa kwajili ya operesheni na hata baada ya
operesheni hutumika.
·
Trimethoprim
Hii dawa hupatikana katika muunganiko au pekee ake. Katika
muunganiko wa dawa hii inajulikana kwa jina la septirini, natumaini hili jina
sio geni kwako. Dawa hii hutumika kutibu UTI na magonjwa yanasababishwa na
wadudu kwenye mfumo wa hewa. Magonjwa kama niumonia.
·
Cefotetan
Hii dawa hutumika Kama dawa ya kuua wadudu waitwao bakteria
wanaopatikana mwilini, dawa hii hutumika katika mazingira mbalimbali ikiwemo
kuzuia kuingia au kusambaa Kwa wadudu kwa magonjwa anayeandaliwa kwajili ya
operesheni au baada ya kutoka kwenye operesheni. Mbali na hayo, dawa hii
hutumika kutibu magonjwa yasababishwayo na wadudu wafuatao; Bacteroides spp., C.perfringes, E.coli,
H.inflenze na N.gonorrhoeae. Kiujumla dawa hii hutibu magonjwa
yasababishwayo na jamii ya wadudu walioko kwenye kundi lijulikanalo kitaalamu
kama gram negative (-ve) na gram
positive (+ve).
2.
DAWA ZA KUTIBU MIWASHO NA
DALILI ZOZOTE ZINAZOHUSIANA NA ALEJI .
Dawa nyingi (sio zote) zinazotumika kuondoa au kutibu
matatizo yoyote yanayohusiana na aleji, utendaji kazi wake huhusisha hadi mfumo
wa kati wa fahamu (ubongo) kwa
kitaalamu unaitwa central nervous system (CNS). Moja ya madhara yanayosababishwa
na hizi dawa ni kupunguza uwezo na umakini kwenye ufanyaji kazi wa ubongo hivyo
kusababisha dalili kama vile usingizi na kupungua kwa ufanisi kwenye kazi.
Hivyo basi, kwasababu
pombe nayo husababisha madhara yanayofanana na yale ambayo yanasababishwa na dawa
za kutibu aleji au miwasho yoyote (Anti-allergy), kwahyo kutumia pombe pamoja
na hizi dawa inaongeza hatari ya kupunguza utendaji kazi wa ubongo na hata
inaweza kupelekea madhara hatari zaidi kama vile kupoteza fahamu au kuzimia.
Dawa zifuatazo ndio zinazotumika kutibu au kuondoa miwasho
mwilini, mpangilio wa orodha hii ya dawa za kutibu aleji umewekwa kwa mtindo
kupungua uwezo wa kusababisha madhara yaliyotajwa hapo juu. Orodha yenyewe ni
kama ifuatayo;
·
Bronpheniramine
·
Chorpheniramine
(piritoni)
·
Ciproheptadine
·
Diphenhydramine
·
Doxylamine
·
Promethazine
·
Acrivastine
·
Cetirizine
·
Levocetirizine
Hivyo basi, ni jambo
la muhimu sana kujiepusha na pombe uwapo katika dozi inayohusisha dawa moja au
mbili zilizotajwa hapo huu. Pamoja na hayo, pombe imehusishwa na kusababisha
kuharibika au kupungua kwa utendaji kazi wa ini ambalo linashughulika na uvunjaji wa dawa na sumu zote
zinazoingia mwilini. Hivyo basi, utumiaji wa pombe kwa muda mrefu unaweza
kusababisha kukusanyika kwa kiasi au kiwango cha sumu mwilini kitu ambacho
kinaweza kusababisha madhara makubwa zaidi mwilini na hata kusababisha madhara
kwenye viungo vingine kama figo. Hivyo basi uwapo katika dozi ya dawa yoyote ni
vyema kupunguza kuacha kabisa unywaji wa pombe hadi umalize dozi yako.
Pia pombe inauwezo
wa kuchochea uvunjaji wa dawa mwilini (enzyme inducer), uvunjaji huu wa dawa
unapochochewa unapelekea kupungua kwa kiwango cha dawa kinahitajika kusababisha
matokeo chanya kwenye kutibu matatizo mbalimbali ya mwili.
Basi, ni jambo jema
na la busara kumshirikisha mfamasia au daktari aliyekuhudumia ili akupatie
maelezo au tahadhari zozote zinazohitajika kuzifahamu wakati wa kutumia dawa na
pombe ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza baada ya kutumia. Ahsante sana kwa
kutumia muda wako kusoma Makala hii.
Usisite kutupatia
mchango wako wa mawazo au kama unaswali lolote usisite kuuliza, tutakupatia
majibu sahihi. Usisahau kumshirikisha mwenzako ili naye apate kuelimika.
Comments